Ushuru wa Trump waanza kuwanyoosha Wamarekani, dunia nayo yalia

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press, Wakati wa kufunga masoko siku ya Ijumaa, Dow Jones Industrial Average ilikuwa imeporomoka kwa asilimia 5.5, Nasdaq Composite ilikuwa chini kwa asilimia 5.8, na S&P 500 ilishuka karibu asilimia 6.

Apr 5, 2025 - 14:29
 0  5
Ushuru wa Trump waanza kuwanyoosha Wamarekani, dunia nayo yalia

Washington. Zikiwa zimepita siku mbili tangu Rais wa Marekani, Donald Trump atangaze kuziwekea nchi zote duniani ushuru wa kuanzia asilimia 10 hadi 50, Masoko ya hisa nchini Marekani yameshuhudia siku nyingine ya hasara kubwa huku ushuru uliowekwa na Rais Trump ukiendelea kusababisha hali ya kutotabirika kwa uchumi wa dunia.

 Miongoni mwa taarifa za mwenendo wa masoko ya hisa nchini Marekani ulionyesha kuporomoka kama unavyoelewa kwamba biashara ya hisa hutegemea ushirikiano wa wadau kutoka ndani ya Nje ya nchi husika. Hivyo kitendo cha kuweka ushuru huo kimeathiri hata makampuni ya hisa ya Marekani.

 Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press, Wakati wa kufunga masoko siku ya Ijumaa, Dow Jones Industrial Average ilikuwa imeporomoka kwa asilimia 5.5, Nasdaq Composite ilikuwa chini kwa asilimia 5.8, na S&P 500 ilishuka karibu asilimia 6.

 Kwa ujumla, viashiria hivyo vitatu vilishuhudia kuporomoka kwa siku mbili kulikokuwa mbaya zaidi tangu Machi 2020, wakati madhara ya kiuchumi ya janga la COVID-19 yalipoanza kuonekana.

 Kuporomoka huko kulifuata tangazo la Trump siku ya Jumatano kuhusu ushuru mpana wa kulipiza kwa karibu washirika wote wa kibiashara ikiwemo ushuru wa msingi wa asilimia 10 kwa washirika wengi, na ushuru maalum uliopanda hadi asilimia 50 kwa zaidi ya nchi 60.

 Akiripoti kutoka Soko la Hisa la New York, mwandishi wa Al Jazeera Kristen Saloomey alisema kuanguka kwa masoko siku ya Ijumaa kulichochewa pia na tangazo la China la kutoza ushuru wa asilimia 34 kwa bidhaa za Marekani kulipiza kisasi kubwa zaidi hadi sasa.

 “Hii yote imechochea hofu ya vita vya kibiashara vya kimataifa na uwezekano wa mdororo wa uchumi wa dunia, na ndiyo tunaona ikijitokeza kwenye masoko leo,” alisema.

 Kwa upande wake, Trump alibakia na msimamo mkali huku akihudhuria mashindano ya gofu ya LIV kwenye uwanja wake wa Florida baada ya kulala usiku katika jumba lake la Mar-a-Lago.

 “KWA WAWEKEZAJI WENGI WANAOINGIA MAREKANI NA KUEKEZA FEDHA NYINGI SANA, SERA ZANGU HAZITABADILIKA KAMWE,” aliandika katika mtandao wa Truth Social, ambao ni mali yake.

 Pia alisifia ripoti mpya inayoonyesha kuwa Marekani iliongeza ajira 228,000 mwezi Machi – zaidi ya matarajio – ingawa ripoti hiyo ilihusisha kipindi kabla ya ushuru mpya kutangazwa.

 “KAA IMARA, HATUWEZI KUSHINDWA!!!” aliandika.

 Tukio la Trump kuhudhuria tamasha la burudani wakati masoko yakiporomoka halikupita bila kutajwa na wakosoaji wake. Kiongozi wa Wademokrasia katika Seneti, Chuck Schumer, alisema rais alikuwa kwenye “bubble ya mabilionea.”

 Seneta Ben Ray Luján, kutoka chama cha Democrats, alisema, “Wakati Wamarekani wanahangaika kuweka chakula mezani, naona Trump yuko huko anacheza gofu.”

 Wakati huo huo, baadhi ya Warepublican waliendelea kumtetea Trump, huku Seneta John Barrasso akimsifu kuwa ni “mtaalamu wa mikataba” ambaye “atapanga mikataba na kila nchi moja kwa moja.”

 Siku hiyo ngumu kwenye ‘Wall Street’ ilikuja huku Mwenyekiti wa Hifadhi ya Shirikisho (Fed), Jerome Powell, akitabiri kuongezeka kwa mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira kutokana na mpango wa ushuru wa Trump kuwa “mkubwa kuliko ulivyotarajiwa.”

 “Tunakabiliana na hali ya kutotabirika sana yenye hatari kubwa ya mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira kuongezeka,” aliwaambia waandishi wa habari.

 Powell pia alivunja matumaini kuwa Fed inaweza kuchukua hatua haraka kupunguza athari hizo ikiwa ni pamoja na ombi la Trump, ambaye aliandika kwenye Truth Social kuwa “huu ndiyo wakati mzuri” wa kushusha viwango vya riba.

 Powell alisema ni mapema mno kuamua ni hatua gani benki kuu ichukue.

 Wakati huo huo, dunia iliendelea kutoa maoni kuhusu ushuru huo.

 Kamishna wa Biashara wa Umoja wa Ulaya, Maros Sefcovic, alisema alimwambia Waziri wa Biashara wa Marekani, Howard Lutnick, na Mwakilishi wa Biashara, Jamieson Greer, kuwa ushuru wa asilimia 20 dhidi ya Umoja wa Ulaya ni “mbaya” na “hauna msingi.”

 “Uhusiano wa kibiashara kati ya EU na Marekani unahitaji mwelekeo mpya. EU imejitolea kwa mazungumzo ya maana lakini pia iko tayari kulinda maslahi yetu. Tutaendelea kuwasiliana,” aliongeza.

 Umoja wa Mataifa pia ulizungumzia sera ya ushuru ya Trump, ambayo imeathiri sana nchi masikini barani Afrika na Kusini-Mashariki mwa Asia zinazotegemea ushuru kuingiza mapato ya serikali.

 Nchi kama Lesotho, Madagascar na Laos zilipigwa ushuru mkubwa zaidi na utawala wa Trump, ambao ulihesabu viwango vya ushuru kwa kugawanya mara mbili kile nchi husika zinachotoza kwa wauzaji bidhaa wa Marekani.

 Mabadiliko haya ya kibiashara “yanaumiza walioko hatarini na masikini,” alisema Katibu Mkuu wa UN wa Biashara na Maendeleo, Rebeca Grynspan.

 “Biashara haipaswi kuwa chanzo kingine cha misukosuko. Inapaswa kusaidia maendeleo na ukuaji wa uchumi wa dunia,” alisema.

What's Your Reaction?

Like Like 1
Dislike Dislike 0
Love Love 0
Funny Funny 0
Angry Angry 0
Sad Sad 0
Wow Wow 0