Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, dereva wake wafariki dunia
Mhandisi, Gisima Nyamohanga na dereva wake walikuwa wakitokea mkoani Mwanza kwenda mkoani Mara kabla ya kupata ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia leo wilayani Bunda mkoani Mara.
Mara. Mkurugenzi wa Shirika la Usambazaji Umeme nchini (TANESCO), Mhandisi, Gisima Nyamohanga na dereva wake wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajali iliyotokea wilayani Bunda mkoani Mara.
Taarifa ya kifo cha wawili hao imethibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi ambaye amesema tukio limetokea kati ya saa 6 hadi 7 usiku.
"Ni kweli tukio lipo na amefariki dunia ila wasiliana na RPC atakuwa na taarifa kwa kina," amesema Mtambi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, RPC Pius Lutumo, tukio hilo limetokea baada ya gari la Mkurugenzi lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Bunda kugongana uso kwa uso na lori.
Amesema chanzo cha tukio hilo ni dereva wa gari lililokuwa limembeba Mkurugenzi aina ya ‘Landcruser’ kumkwepa mwendesha baiskeli na kupoteza muelekeo kisha kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa mbele yao.
"Tukio limetokea Bunda saa 7.30 usiku baada ya derava wa gari dogo kumkwepa mwendesha basikeli na kugongana uso kwa uso na lori kisha kupelekea vifo vya dereva na bosi wake," amesema RPC Lutumo
Naye, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mara, Nickson Babu amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali Teule ya wilaya ya Bunda huku wakisubiri taarifa zaidi kuhusu taratibu zingine.
What's Your Reaction?






