Rais Samia atoa kauli kifo cha Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, dereva wake

Mhandisi, Gisima Nyamo-Hanga na dereva wake walikuwa wakitokea mkoani Mwanza kwenda mkoani Mara kabla ya kupata ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia leo wilayani Bunda mkoani Mara.

Apr 13, 2025 - 12:04
 0  5
Rais Samia atoa kauli kifo cha Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, dereva wake
Rais Samia Suluhu Hassan

Mara. Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kufuatia kifo cha 
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamohanga na dereva wake, Mohammed Haule.

Katika taarifa yake Rais Samia ameandika:

“Nimepokea kwa masikitiko
taarifa ya vifo vya Mhandisi Boniface Gissima Nyamohanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), pamoja na dereva wake, Muhajiri Mohammed Haule, vilivyotokea usiku wa kuamkia leo kwa ajali ya barabarani eneo la Bunda, Mkoa wa Mara.”

“Ninatoa pole kwa familia, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, watumishi wa TANESCO, ndugu jamaa na marafiki. Namuomba Mwenyezi Mungu azijaalie familia, ndugu, jamaa na marafiki subra, uvumilivu na moyo wa ibada katika kipindi hiki kigumu.
Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi.Amina.”

Taarifa ya kifo cha wawili hao imethibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi ambaye amesema tukio limetokea kati ya saa 6 hadi 7 usiku.

"Ni kweli tukio lipo na amefariki dunia ila wasiliana na RPC atakuwa na taarifa kwa kina," amesema Mtambi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, RPC Pius Lutumo, tukio hilo limetokea baada ya gari la Mkurugenzi lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Bunda kugongana uso kwa uso na lori.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni dereva wa gari lililokuwa limembeba Mkurugenzi aina ya ‘Landcruser’ kumkwepa mwendesha baiskeli na kupoteza  muelekeo kisha kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa mbele yao.

"Tukio limetokea Bunda saa 7.30 usiku baada ya derava wa gari dogo kumkwepa mwendesha basikeli na kugongana uso kwa uso na lori kisha kupelekea vifo vya dereva na bosi wake," amesema RPC Lutumo

Naye, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mara, Nickson Babu amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali Teule ya wilaya ya Bunda huku wakisubiri taarifa zaidi kuhusu taratibu zingine.

What's Your Reaction?

Like Like 0
Dislike Dislike 0
Love Love 0
Funny Funny 0
Angry Angry 0
Sad Sad 0
Wow Wow 0