Dodoma. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2000 hadi 2025, Serikali ya Tanzania anayoingoza imetekeleza yote iliyoagizwa kuhusiana na mhimili wa Mahakama, na hata zaidi.
Rais Samia amesema Serikali haina deni tena na mhimili wa Mahakama nchini huku akiutaka kuchapa kazi na kuwahudumia watanzania.
“Ukiangalia kazi iliyofanywa katika mhimili wa Mahakama, ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi tumefanya zaidi ya tulivyoagizwa. Ukisoma Dira ya Taifa 2000 hadi 2025, yote tuliyoagizwa tayari serikali tumeyatekeleza. Kwa maneno ya vijana wa siku hizi, hatudaiani, hatudaiani,” amesema Rais Samia.
Rais samia ametoa kauli hiyo leo Aprili 5, 2025, katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama, Jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na jengo la makazi ya Majaji, jijini Dodoma.
Rais Samia amesisitiza kuwa sasa ni zamu ya Mahakama kufanya kazi kwa ufanisi, kwani upande wa serikali tayari umemaliza wajibu wake.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema kuwa jengo jipya la Mahakama Kuu litafanya kazi na kutoa huduma bila kutumia karatasi, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa haki kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Amesema kuwa jengo hilo jipya litatumika kuendesha shughuli za kimahakama kwa mfumo wa kidijitali, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi na uwazi katika shughuli za utoaji haki.
"Tumearifiwa kuwa mahakama hii tunayoizindua leo inakwenda kutoa huduma bila karatasi, yaani paperless, ni mambo ya mtandao na teknolojia ndiyo yatatawala humu ndani," amesema Rais Samia.
Hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi makubwa katika mfumo wa mahakama nchini, ambapo jengo hilo la Mahakama Kuu, mbali na kutumia huduma za kisasa, linatajwa kuwa la kwanza kwa ukubwa barani Afrika na la sita kwa ukubwa duniani.