Iran yasema iko tayari kwa vita na Marekani, yasema ‘msitupangie’

Kauli ya Araghchi imetolewa leo Jumapili Aprili 6,2025, kupitia taarifa, baada ya Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, kusema mwezi uliopita kupitia barua aliyomtumia Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, kwamba alitumaini kuwepo kwa mazungumzo kati ya mataifa hayo ili kuzuia Tehran kupata silaha za nyuklia.

Apr 6, 2025 - 19:28
 0  3
Iran yasema iko tayari kwa vita na Marekani, yasema ‘msitupangie’
Iran yasema iko tayari kwa vita na Marekani, yasema ‘msitupangie’

Tehran. Licha ya kulimwa vikwazo vilivyochangia kuporomoka kwa sarafu yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na Marekani hautowezekana kwani mazungumzo hayo hayana maana tena hususan wakati huu ambao mvutano kati ya nchi hizo unazidi kuongezeka.

Kauli ya Araghchi imetolewa leo Jumapili Aprili 6,2025, kupitia taarifa, baada ya Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, kusema mwezi uliopita kupitia barua aliyomtumia Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, kwamba alitumaini kuwepo kwa mazungumzo kati ya mataifa hayo ili kuzuia Tehran kupata silaha za nyuklia.

Trump aliongeza kasi ya matamshi wiki iliyopita kwa kusema: “Wasipokubaliana kufanya makubaliano, kutakuwa na mabomu.”

Araghchi amehoji uaminifu wa Marekani katika wito wake wa mazungumzo, akisema Jumapili: “Kama kweli mnataka mazungumzo, basi lengo la vitisho ni nini?”

Tehran, ambayo inasisitiza kuwa haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia, hadi sasa imekataa mikakati ya wazi ya Washington, lakini imesema iko tayari kwa diplomasia ya moja kwa moja kupitia njia zisizo za moja kwa moja msimamo ambao Araghchi alirudia katika taarifa yake ya Jumapili.

Araghchi amesema Iran inataka kufanya mazungumzo kwa “masharti sawa” na Marekani, akiitaja Marekani kuwa ni “mhusika ambaye mara kwa mara hutishia kutumia nguvu kinyume na Katiba ya Umoja wa Mataifa, na ambaye maofisa wake hutoa kauli zinazokinzana.”

Kuongeza shinikizo

Nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani, zimekuwa zikiishutumu Iran kwa miongo kadhaa kwa kutaka kutengeneza silaha za nyuklia.

Mnamo mwaka 2018, wakati wa muhula wake wa kwanza, Trump alivunja Makubaliano ya Pamoja ya Nyuklia (JCPOA), ambayo yalikuwa kati ya Iran na wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo yalipatia Iran nafuu ya vikwazo kwa masharti ya kupunguza shughuli zake za nyuklia.

Tangu wakati huo, Iran imeanza kurudi nyuma katika utekelezaji wa makubaliano hayo, na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) limeripoti kwamba Iran imekusanya kiasi cha kutosha cha nyenzo za nyuklia kwa ajili ya kutengeneza mabomu kadhaa.

Akijibu tishio la vita kutoka kwa Trump, Hossein Salami, mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), alisema Jumamosi kuwa taifa hilo liko “tayari” kwa vita.

“Hatuna wasiwasi kuhusu vita kabisa. Hatutakuwa waanzilishi wa vita, lakini tuko tayari kwa vita yoyote,” shirika rasmi la habari la IRNA lilimnukuu Salami akisema.

Hata hivyo, msimamo wa Tehran katika ukanda wa Mashariki ya Kati unaonekana kudhoofika, kufuatia vita vinavyoendelea Gaza na maeneo mengine, pamoja na mauaji ya viongozi wa Hezbollah nchini Lebanon na kuondolewa madarakani kwa mshirika mwingine muhimu, Rais wa Syria Bashar al-Assad, mwaka jana.

Iran inasema shughuli zake za nyuklia ni kwa madhumuni ya kiraia pekee. Israel, mshirika mkuu wa Marekani katika eneo hilo, inaaminika kuwa na hazina ya silaha za nyuklia ambayo haijatangazwa rasmi.

Mwisho.

What's Your Reaction?

Like Like 0
Dislike Dislike 0
Love Love 0
Funny Funny 0
Angry Angry 0
Sad Sad 0
Wow Wow 0