Unataka kuandamana? Shehe Kabeke ana ujumbe wako

Wito huo umetolewa na Shehe Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke ambaye amekemea na kuwatahadharisha wananchi kutoingia mtego wa kujiingiza kwenye shughuli zinazoweza kuondoa amani ya nchi hususan ni maandamano.

Mar 28, 2025 - 00:04
Mar 31, 2025 - 14:53
 1  15

Mwanza. Waumini wa dini ya Kiislamu nchini wametakiwa kutotumika kisiasa kuondoa amani ya nchi badala yake washiriki kwa kufanya siasa safi zisizoleta mtengano katika jamii.

Wito huo umetolewa na Shehe Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke ambaye amekemea na kuwatahadharisha wananchi kutoingia mtego wa kujiingiza kwenye shughuli zinazoweza kuondoa amani ya nchi hususan ni maandamano.

“Niwaase watanzania tuienzi amani hususan waislamu, dini yenu ni dini ya amani, unyenyekevu ndiyo maana ikaitwa al-Islam. Ukikutana na mtu akaanza kukupigia maneno bila kukuhakikishia amani usimjibu, mwambie tu Assalam Alykum,” amesema Shehe Kabeke.

 Shehe Kabeke amewataka wananchi kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uchaguzi huo kuanzia kujiandikisha, kuchukua fomu ya kugombea na kupiga kura bila kuchochea vurugu za aina yoyote.

 Kabeke amewataka waislamu kuendeleza matendo mema waliyojifunza wakati wa siku 30 za mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan sambamba na kuendeleza ibada kama walivyokuwa wakifanya katika kipindi chote cha mfungo.

Kauli ya Shehe Kabeke imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Ramadhan Charity Program, Ahmed Missanga ambaye amedai kubaini uwepo wa uhitaji wa msaada katika jamii iliyoguswa na taasisi hiyo kwa siku 30 za mfungo huo. Missanga amesema kupitia Sadaka na Iftar iliyotolewa mwezi wa ramadhani kwenye vituo 420 mikoa sita ya Kanda ya Ziwa, amebaini kuwa familia zilikuwa zikishindia mlo mmoja ama maji na tende jambo linalotoa taswira kuwa ni wajibu waumini wa dini hiyo kuendelea kusaidia wenye uhitaji.

“Nitoe rai moja kwamba Ramadhani imekuwa chuo cha mafunzo, watu wakaiishi kwa wema sana walifanya mema sana na kutoa misaada na kusaidia maskini, wajane na yatima. Watu walifanya ibada na kusoma Quran tukufu, niwakumbushe kwamba tukaendeleze matendo hayo,” amesema Missanga.

Amewataka wananchi bila kujali imani zao kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola wanapobaini vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani hususan kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Mkazi wa Mkuyuni jijini Mwanza, Husna Ally amesema kupitia mfungo huo, amejifunza kuwajali wenyr uhitaji na kuendeleza amani kuanzia ngazi ya familia hadi kwenye jamii. “Tunawajibu wa kuendeleza amani katika familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu tunatambua wanasiasa watakuja na mbinu mbalimbali tuwazingatie wenye hoja za kujenga. Wanalenga kutuhamasisha kuondoa amani tukawapuuze,” amesema Husna.

Kwa upande wake, Mkazi wa Isamilo jijini Mwanza, Munah Mussa amesema kupitia mfungo na ibada ya leo amejifunza kumrejea Mungu kwa kufanya matendo mema ndani ya jamii ikiwemo kutoa zaka na sadaka.

What's Your Reaction?

Like Like 2
Dislike Dislike 0
Love Love 1
Funny Funny 0
Angry Angry 0
Sad Sad 0
Wow Wow 0