Ahmed Ally atoa kauli ya kuiua Al Masry

Mchezo huo utapigwa Jumatano Aprili 9,2025, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa (Kwa Mkapa) kuanzia Saa 10:00 alasiri.

Apr 5, 2025 - 16:32
 0  8
Ahmed Ally atoa kauli ya kuiua Al Masry
Afisa habari wa club ya Simba akizungumza na waandishi wa habari

Dar es Salaam. Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Wekundu wa Msimbazi (Simba), Ahmed Ally amesema Klabu ya Al Masry ‘itake isitake’ Klabu ya Simba itasonga mbele hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAFCL).

 Simba ilipoteza dhidi ya Al Masry, nchini Misri kwa mabao 2-0 ambapo itakuwa na kibarua cha kupindua meza kwa kufunga mabao angalau 3-0 nyumbani ili iweze kufuzu moja kwa moja.

 Akizungumza leo katika moja ya Mikita no ya hamasa jijini Dar es Salaam, Ally amesema Simba haina chaguo lingine katika mchezo huo zaidi ya kupata ushindi wa kishindo utakaoiwezesha kufuzu moja kwa moja hatua ya nusu fainali.

 “Tunataka kwenda Nusu Fainali, Al Masry watake tutaenda wasitake tutaenda. Wavinga macho watake tutaenda, wavimba macho wasitake tutaenda safari hii hatuishii robo fainali. Tutasema kwa nguvu moja na sauti moja hii tunavuka,” amesema Ally.

 Mchezo huo utapigwa Jumatano Aprili 9,2025, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa (Kwa Mkapa) kuanzia Saa 10:00 alasiri.

 Meneja huyo amesema awali kwenye michuano hiyo ya Kimataifa Tanzania ilikuwa ikiwakilishwa na timu nne ambazo ni Yanga, Simba, Azam na Singida Black Stars huku akisema timu ‘goigoi’ zote zimeshatolewa kwenye michuano hiyo.

 “Amebaki Simba SC pekee nafahamu kwamba wanaumia Simba kuwa hapa na Simba kuichungulia nusu fainali wanatamani kufanya kila hila ili mnyama aishie hapa robo fainali sasa tuwaambie yoyote ambaye atatia mikono kwenye Machi ya tarehe 9 aache ameandika wosia kabisa kwenye familia yake,” amesema Ally.

Kwa upande wake Shabiki wa Simba kutoka Mnazi Mmoja jijini humo, Salum Mohamed amesema anaamini warabu watafungwa mabao zaidi ya matatu katika mchezo huo.

 “Hawa waarabu wamekuwa wakija Benjamin Mkapa wanapasuka Mara zote. Naamini hata hawa Al Masry tutawapasua vizuri tu,” amesema Mohammed.

Anna Johnson amesema anaiombea Simba ishinde mchezo huo ili iendelee kuiwakilisha nchi katika michuano hiyo.

What's Your Reaction?

Like Like 2
Dislike Dislike 0
Love Love 0
Funny Funny 0
Angry Angry 0
Sad Sad 0
Wow Wow 0